Ticker

6/recent/ticker-posts

Hizi ndizo changamoto sita za uongozi..

Uongozi ni sifa ambayo kila mtu angependa kuwa nayo katika maisha, na uongozi huo unaweza ukawa katika maeneo mbalimbali kama vile katika masuala ya kiafya, kisiasa, maendeleo binafsi na kadhalika. Katika maisha kila mtu ni kiongozi na hauitaji kuwa na cheo ndio utambulike kuwa kiongozi, yaani mpaka sasa wewe tayari ni kiongozi. Jinsi unavyoyaishi maisha yako ndivyo unavyoyaongoza maisha yako (uongozi). Na katika makala yetu ya leo tutaangalia changamoto mbalimbali za uongozi hasa linapokuja suala la kuwaongoza wengine. Zifuatazo ni changamoto  sita za uongozi..

Kukataliwa ; changamoto ya kwanza utakayokumbana nayo katika uongozi ni ile hali ya kukataliwa. Ikiwa upo tayari kuitikia wito wa kuwa kiongozi, basi ni muhimu ukatambua kwamba kuna wakati utakumbana na hali ya kukataliwa ama kutokueleweka kwa wale unaowaongoza.  Kama kitu unachopanga kufanya watu watakikataa, hivyo utajikuta unakata tamaa ya kuendelea na uongozi na kuhisi kukataliwa pia kihisia. Na hiyo itasababisha kuogopa kabisa kuweka mipango na mikakati yako ya kiuongozi na matokeo yake kupeleka kuwa na uongozi mbaya. Kwa hiyo hapa jambo la muhimu ni wewe kama kiongozi unatakiwa ujiamini na usikubali kukata tama sababu kukataliwa ni sehemu tu ya changamoto za uongozi  kama ilivyo pia katika maisha.


Upinzani na kukosolewa; Changamoto nyingine utakayokumbana nayo pale utakapoamua kujihusisha na masuala ya uongozi ni kupata upinzani ama kukosolewa katika kila utakachokuwa unakifanya. Na kama tujuavyo kwamba uongozi unahusisha kufanyika kwa maamuzi na kuamua mwelekeo. Sasa basi katika kila maamuzi utakayokuwa ukiyafanya tarajia kukutana ama kukumbana na mwitikio au majibu kutoka kwa wale  unaowaongoza. Na mwitikio huo unaweza ukawa ni hasi au chanya.

Upweke; Wakati mwingine kujiingiza katika uongozi ni sawa na kujiingiza katika hali ya upweke, kwa sababu ni lazima utatakiwa uwe mbele zaidi ya wafuasi wako katika kila jambo. Na pia ni kwa sababu kiongozi ni mtu anayeongoza maono (mwenye dira) na dhumuni la lengo husika, anakuwa anauona mwisho kutoka mwanzoni na ni lazima ajitoe kikamilifu katika kukamilisha mchakato, au kiongozi ndiye mtu pekee anayepanga mwelekeo na kuwaongoza wengine ili waweze kufikia malengo.

Shinikizo na kutatizwa; Kiongozi ni lazima akumbane na changamoto za wajibu na mahitaji mbalimbali yatokanayo na uongozi. Majukumu au mahitaji hayo ni kama vile; hitaji la kufanya maamuzi magumu, na mara nyingi huwa chini ya vikwazo na shinikizo la nje.

Uchovu wa akili na kimwili; suala la uchovu wa kimwili na kiakili ni moja ya  changamoto kwa kila kiongozi sababu katika uongozi utahitajika kutimiza majukumu makubwa na madogo kwa kutumia mwili na akili yako. Na hali hiyo itapeleka kuchoka kiakili sababu uongozi unahitaji akili ya mtu katika kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi, kushauri na kuandaa mipango bora ya kiuongozi. Na pia uongozi utasababisha kuwepo kwa msongo wa mawazo.
Gharama itakayolipwa na walio karibu yako; lazima ufahamu gharama na changamoto kubwa itakayozaliwa kutoka kwa wale waliopo karibu yako (kama vile familia yako). Sababu uongozi unahitaji kujitoa kwa ajiri ya  wengine, na maisha yako yatakuwa ni mali kwa wale unao watumikia.
Nakutakia wakati mwema na TUPO PAMOJA.

Makala hii imeandikwa na  Geofrey Mwakatika.Unaweza kusoma makala zake nyingi zaidi za kuhamasisha na kuelimisha kwa kutembelea mtandao wake kwa kubonyeza hapa ( GEOFREY MWAKATIKA)