"HISIAHISIA KATIKA MAAMUZI NA MAFANIKIO"
Hisia ni msukumo wa ndani ya mwili au akili ambao huweza kusababisha matendo hasi au chanya kwa mhusika. Matendo hayo ni kama, hasira, furaha, huzuni, sononeko, kero, kijicho, wivu n.k. Hisia ni muhimu katika maisha ya binadamu maana ndizo hufanya maisha yake yaendelee. Mfano; Hasira ina umuhimu katika maisha ya binadamu maana humfanya aweza kujilinda hivyo kuendeleza maisha, Pamoja na hilo ila lazima uwe na uwezo wa kuthibiti hasira yako vinginevyo utakufa kabla ya umri wako.Tunapaswa kutumia vizuri hisia zetu ili ziwe msaada kwetu na kwa wengine badala ya kuwa maumivu kwetu na kwa wengine.
"Unapokuwa unafanya maamuzi yatakayoamua hatima ya maisha yako usifuate hisia"
Maumivu mengi na kushindwa kwetu kimaisha kunatokana na kushindwa kwetu kuzipeleka mahali bora hisia zetu ili zisitupe maumivu na badala yake ziwe na msaada kwetu. Kwa mfano: upande wa pili wa kijicho ni wa kujenga. Badala ya kuwa na hasira na kulaani na kumshusha aliyefanikiwa, mtu anaweza kujiambia kumbe inawezekana, na mimi nitajitahidi. Hapa ni kijicho kilekile ila kimegeuzwa kuwa wivu wa maendeleo (kutoa nafasi na muda kwenye kijicho katika mkabala wenye kujenga).
Mara nyingi hisia huwa ni matokeo ya vile tunavyoviona, tunavyopitia (experience), mambo yaliyopita, au taswira za mambo yajayo. Unaweza kuwa na hisia ya hofu katika kufanya jambo fulani ambalo unahisi litakuletea manufaa kutokana na maisha ambayo umepitia ambayo yalikufanya ujishisi wewe ujione huwezi tu. Hiyo ni hisia mbaya kabisa.
"Ili ufanikiwe ni lazima hisia za kushindwa zisizidi hisia za kushinda" Robert kiyosaki anasema "Mafanikio ni kuweza kushinda hofu ya kushindwa na kuwa na kuwa na nguvu ya kustahimiri magumu na shida unazokumbana nazo"
Watu wengi waliofanikiwa ukifuatilia utagundua kuwa mafanikio yao yalikuja wakati hisia zao zikiwatuma kuacha walichokuwa wanakifanya lakini wakajipa moyo kujaribu mara ya Mwisho na ndipo walipofanikiwa mara hiyo.
"Th Success always comes at the point of disapointment".
Fursa hazionekani kwa hisia bali huonekana kwa akili. Kama utatumia hisia kutambua fursa itakayokufanya ufanikiwe bila shaka utajikuta unavamia fursa ambayo haiendani na wewe.
Ukimuuliza mkulima na msafirishaji wa mpunga kule mbeya atakwambia hakuna biashara inayolipa na kukufanya utoke haraka kama kilimo na usafirishaji wa mazao. Akikupa takwimu zako unaweza kujiona tajiri ndani ya siku moja na pengine ukatamani kuuza kila kitu uingie katika fursa hiyo.
> Ukikutana na muuza viatu pale karume Dar es salaam atakwambia hapa ndo penyewe ukinunua robota moja tu utapata faida moja mbili tatu na muda si mrefu utakuwa na pesa nyingi zitakazokufanya ufanye kitu cha maana, Kama hutakuwa makini utasimuka kuingia katika biashara hiyo pia.
> Ukienda kwa walima vitunguu huko mang'ora Arusha watakwambia wewe unachelewa njee tupige pesa unajichelewesha bure, vijana wadogo tu wanatusua mamilioni, Bila shaka wakikupa takwimu na mifano ya watu waliofanikiwa kimaisha kupitia shughuli hiyo utasema kweli umechelewa.
> Ukienda kwa wakulima wa tikiti maji kule kigamboni wakikusimulia kuwa wanapata milioni 9 kwa ekari bila shaka hapo utashawishika kuingia huko pia.
Uchaguzi ambao utaufanya pindi unapoona fursa ndio utakaoashiria ukubwa wa mafanikio utakaofikia.
Kuna tofauti mbili katika maamuzi kati ya mtu aliyefanikiwa na asiyefanikiwa: moja, Mtu mwenye mafanikio huwa hafuati hisia zake pekee katika kufanya maamuzi wakati mti asiye na mafanikio hufanya masmuzi kwa kufuata hisia pekee au mkumbo,
Pili mtu aliyefanikiwa huchukua maamuzi kwa wakati muafaka pindi fursa inapotokea na bila kukurupuka wakati mtu asiye na mafanikiwa hukurupuka katika maamuzi yake ama husitasita katika kufanya maamuzi na mwishowe hujikuta amechelewa.
"Choose wisely for the future betterment"
Mara nyingi katika Maisha tunalazimika kufanya uchaguzi baina ya vitu viwili au zaidi. Kiuhalisia kufanya maamuzi siyo jambo rahisi kwa sababu kila kitu unachokichagua kitaacha Alama katika Maisha yako. Ni rahisi sana pindi unapokuwa unafanya uamuzi kujikuta unafuata hisia badala ya kuangalia vitu vya msingi kuhusu uchaguzi unaofanya.
"Kuiona fursa ni jambo moja lakini kutambua fursa bora na kufanya uamuzi ni jambo lingine"
> Ili uweze kufanya maamuzi sahihi baada ya kuiona fursa unatakiwa kuchukua hatua zifuatazo badala ya kufuata hisia au mihemuko:
1. Kaa chini utulie Kisha anza kuichambua fursa hiyo. "Usikurupuke".
Watu wengi hufanya maamuzi mabaya kwa sababu wanakurupuka na hawafikirii vizuri kuhusu matokeo ya maamuzi hayo.
Kuwa na hali ya utulivu na na kuchambua kila wazo kwa kichwa kilichotulia ni mwanzo mzuri katika maamuzi. Chukua muda kidogo kufanya uchaguzi sahihi lakini usisahau kuwa hakuna mtu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia 100, kwamba wajati mwingine unaweza kufanya maamuzi ambayo ni hatarishi kabisa lakini hiyo haimanishi kuwa ndiyo mwisho wa maisha. Japokuwa wakati mwingi maamuzi unayofanya hayawezi kuja kubadilika baadaye. Fikiria kwa makini kuwa maamuzi hayo yatakupeleka wapi katika siku za mbeleni zaidi kuliko kufikiria matokeo ya leo na kesho tu. Hii hatua ni muhimu sana hasa unapokuwa unashughulika na kesi ambayo inaenda kubadili maisha yako kwa ujumla, kama vile kuoa au kuolewa.
2. Uliza au wataarifu watu wengine.
Kuwataarifu wengine hukusaidia kupanga mawazo yako vizuri. Pindi unapokuwa umechanganyikiwa au kusisimuka kupitiliza kuhusu fursa uliyoisikia au kuiona, Kuongelea Fursa hiyo na na matokeo yake vinaweza kukurudishwa katika njia sahihi. ..
> Wataarifu watu ambao unawaamini. Kama unaona jambo linakuchanganya na unashindwa kufika kufikia mwafaka ni vyema kuwasiliana na watu ambao wanaaminika, wanaweza kuwa wazazi au marafiki zako wa karibu.Ha ndio msaada wako, ndio mkono wako wa msaada hivyo sikiliza na uthamini mawazo yao.
> Pia ni vizuri ukauliza watu ambao unahisi wamepitia njia kama unayopitia. Lakini ni lazima ukakumbuka kuwa "Hakuna maamuzi au mazingira yanayofanana siku zote, Lakini unaweza kupata uzoefu mkubwa kutoka kwao"
3. Orodhesha machaguo yote ambayo unaweza kuyachukua ili uweze kuyapangilia na kuyachuja.
*** Ondoa mapendekezo au machaguo kwa kuzingatia ubora.
> Fikiria kuhusu kile unachokitaji na uondoe mapendekezo ambayo hayaendani na wewe. Usihofu kutafita ambayo ni nzuri zaidi. Kitu cha msingi unapochagua iliyobora zaidi ni kujiamini na kuamini bila wasiwasi wowote kwamba ipo inayokufaa zaidi wewe.
4.Fikiria kuhusu Faida na hasara za kila uchaguzi.
Hatua hii ni muhimu katika kufanya maaumuzi yoyote. Kwa sababu unajua faida na hasara za kila uamuzi, itakua ni juu yako sasa na urawajibika kwa matokeo ya Uamzi huo. Kumbuka kuwa faida na hasara ni kama sehemu mbili za shilingi, na kila uamuzi unafaida na hasara zake. Cha muhimu ni kuchukua uchaguzi ambao unafaida kwako zaidi.
"Ukifanya uchaguzi uchaguzi huo utakuchagua wewe pia"
"Fanya uchaguzi sahihi ukizingitia matokeo ya uchaguzi huo kwako na kwa watu wengine wanaohusika"
5. Usifikirie kupita kiasi.
Ni vizuri kufikiria kuhusu matokeo ya uamuzi lakini sio kufikiri kupita kiasi na badala yake fikiria changamoto ambazo ni kubwa tu na usonge mbele. Kufikiria kupita kiasi kuhusu uamuzi iliofanya kunaweza kukupa hofu na kusababisha upotevu wa muda na nguvu.
> Unaweza kujiuliza maswali machache tu ya msingi:
* Nini kitatokea ikiwa nitaendelea na uamuzi wangu?
** Nitafaidikaje na uamuzi huu?
*** Nini kitatokea kama mambo hayataenda vizuri? N.k
Baada ya kutosheka na uchaguzi wako fanya maamuzi mara moja bila kupoteza muda.
MWISHO.
Jeffrey R Anderson Anasema “Tazama moyo na nafsi yako kwanza kabla hujatazama kichwa chako, Lakini unatakiwa uchukue kile unachofikiri kuliko kile unacho hisi. Angalia pia asili ya mambo Na Uyahisi maamuzi yako maana ndiyo yatakayobadili maisha yako ya baadaye"
Ndugu msomaji, Unapofanya maamuzi usifuate hisia maana hisia ni za muda mfupi na zikishaisha utakuja kujilaumu kwa uchaguzi au uamuzi wako ambao ulifanya kwa kwa kufuata hisia.
"Kufanya uamuzi ni kuchagua maisha yako ya baadaye"
LUCAS ROBERT
lucastrngwakwa@gmail.com
"Live an inspired life"
