TAMBUATHAMANI YAKO
Hakuna mtu atakayekuthamini kama wewe mwenyewe hautambui thamani uliyo nayo, wala hakuna atakayetambua thamani uliyonayo bila kumuonesha kuwa wewe ni wa thamani.
Kile ambacho wewe unaona ni cha thamani kwa mwingine kinaweza kuonekana kama takataka inayofaa kutupwa jalalani au kuchomwa moto.
Mfalme Daudi alitamani sana kumjengea Mungu Nyumba ya ibada (hekalu) Katika kipindi cha utawala wake...
Isivyo bahati kwake, Hakufanikiwa kwani Mungu alimzuia kutokufanya hivyo kipindi cha utawala wake, Kutokana na makosa kadhaa ambayo yalikuwa yamejitokeza katika utawala wake ikiwemo, Umwagaji damu kupita kiasi na uzinzi.
Hata hivyo Mungu alimwagiza kuandaa vifaa vyote na Gharama zote ambazo zilihitajika kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Bwana kipindi kitakapofika.
Miongoni mwa vifaa hivyo ilikuwa ni Mawe kwa ajili ya kujenga ukuta wa hekalu...
Mafundi ujenzi (Waashi) na wasanifu majengo walipiga hesabu ya ukubwa na idadi ya mawe yote yaliyohitajika kukamilisha ujenzi wa Ukuta.
Idadi ya mawe yote kwa vipimo vyake yalichongwa vizuri tayari kwa kazi ya ujenzi wa hekalu...
Ufalme wa Daudi ukaisha sasa ukaja ufalme wa Sulemani mwana wa Daudi ambaye ndiye ambaye Mungu aliahidi kuwa atakuja kuijenga nyumba ya Mungu kama ambavyo Mungu aliweka agani na baba yake Daudi...
Ujenzi ukaanza na waashi wakaanza kuyapanga mawe yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili ya hekalu, kila jiwe mahali pake.
Wakati ujenzi ukiwa unaendelea Lilionekana jiwe moja dogo ambalo lilionekana kutokufaa, Na mafundi wakalitupa pembeni.
Watu walipokuwa wakija kutazama ujenzi ulivyokuwa unaendelea walijikwaa katika jiwe hilo ambalo mafundi walikuwa wamelitupa pembeni, Hivyo kila aliyejikwaa alilitupa mbali, na hatimaye likajikuta limefika mbali kabisa na eneo la ujenzi.
Karibu kabisa na kukamilika kwa ujenzi wa hekalu mawe yote yakiwa yamekwisha wekwa mahali pake, ilionekana katika kona moja ya Hekalu hapajakaa sawa, Maana ilionekena kuna jiwe linapungua na pasipo kupatikana hilo jiwe basi Jengo zima lingeweza kuporomoka.
Mafundi wakajiuliza,
"Inawezekanaje jiwe likosekane, wakati hesabu yote ilipigwa vizuri tena kwa umakini mkubwa?"
Ndipo wakakumbuka kwamba kuna ki-jiwe ambacho waliona hakifai wakakitupa pembeni na watazamaji wakakitupa mbali zaidi kwani kilionekana hakifai na kiliwakwaza miguu.
Mara moja wakaagiza jiwe hilo litafutwe mpaka lipatikane, Na lilipopatikana, Lilipowekwa mahali pale ambapo palionekana kupungua lilitoshea vizuri sana.
Ndipo ukaja msemo wa wayahudi
"Jiwe walilolikataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni "
![]() |
Jiwe hilo ambalo linaongelewa hapa ni Yesu ambaye hata waalimu wa dini wa kiyahudi (waashi) walimkataa.
Swala la kukataliwa linaweza kumkuta mtu yeyote hata kama thamani yake ni kubwa, Ni kwa sababu tu wanaomkataa hawajaona thamani ambayo walikuwa wanaitarajia.
Lakini Leo nakuambia wewe unayesoma makala hii, Kama Mungu aliruhusu Uzaliwe na Leo uko hai, WEWE NI WA THAMANI SANA, Na ipo sehemu ambaye unafaa zaidi kuliko mtu mwingine yoyote (hiyo nafasi ni kwa ajili yako tu).
Tambua thamani yako, Tafuta kujua kusudi la Mungu lililopo ndani yako na pambania nafasi ambayo Mungu amekuumba kwa ajili yake.
Usimwangushe Mungu aliyekuumba na kukupatia nafasi ya kuwa hai.
Hata kama watu wote washindwe kutambua thamani yako, Lakini Elewa wewe ni jiwe la thamanj katika nyumba ya Mungu.
Pambana pasipo kukata tamaa
"Live an inspired life"
Imeandaliwa na Lucas Robert
Blog: Fanikiwanaafyayako.blogspot.com
Facebook/Instagram: Fanikiwa_na_afyayako

