UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI.
Ufugaji wa kuku imekuwa ni mojawapo ya shughuli ambayo imekuwa ikifanywa na Familia nyingi Sana hapa Tanzania kwa lengo la kujipatia kipato na mahitaji mengine. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni pamoja na mayai, nyama, mbolea na manyoya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mifumo ya ufugaji kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria na shadidi. Pamoja na kwamba ufugaji wa kuku wa kienyeji hapa nchini umekuwa ukifanywa na familia nyingi, bado hauna tija kwa sababu haufuati kanuni za ufugaji bora.
VITU UNAVYOHITAJI KUVIFAHAMU KABLA YA KUANZA UFUGAJI WA KUKU.
1. Mahitji na Aina ya banda bora
•
2. Kuchagua kuku bora wa kufuga
3. Kutunza na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
4. Kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuku
5. Kutunza kumbukumbu
## 1.BANDA LA KUKU
Banda la kuku lazima liwe bora na liwe safi ili kupusha magonjwa ya kuambukiza kwa kuku.
SIFA ZA BANDA BORA KWA AJILI YA KUKU WA KIENYEJI.
1. Liwe imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
2.Liwe lenye mwanga wa kutosha, hewa safi na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
3.Banda lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
4.Banda liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala.
5. Linatakiwa liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga.
6.Lazima liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na nafasi ya kuweka vyombo vya chakula na maji.
7. Kama ni kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa.
8. Pia Kama ni kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga wa kutosha.
Hayo ndiyo mambo ya kuzingatia katika ujenzi wa banda la kuku ili kufanya ufugaji uwe na tija kwa mfugaji kwa sababu itakusaidia kulinda kuku wako na kuzuia vifo na magonjwa ya kuambukiza kwa kuku wako.
VIFAA VINAVYOTUMIKA KATIKA UJENZI WA BANDA LA KUKU.
Vifaa vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
• SAKAFU: Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
• KUTA: Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
• PAA: Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
• WIGO: Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati
UKUBWA WA BANDA
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina, na njia ya ufugaji.
(a) Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 20 wa umri wa wiki 1 - 4. Hivyo banda lenye mita za mraba 15 linaweza kulea vifaranga 300 hadi wiki 4.
(b) Kuku wakubwa wa mayai 7-9 kwa square metre moja na wa nyama 9-10 kwa square metre moja
ina maana kuku mia tano ni banda (500kuku/10)= 50m2 approx 5mx10m au kipimo chochote upate 50m2 hii kwa broiler wanahitaji layers kwa sababu ya viota na pia sababu wataishi muda mrefu wanahitaji nafasi zaidi kuweza kufanya mazoezi (hawahitaji uzito mkubwa)
kuku 500/9 = 55.5m2 approx 5mx11m
Pia nafasi inategemea mzunguko wa hewa, kama huna space au umebanwa usijaze kuku ili kuepuka vifo kwa magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
## 2. KUCHAGUA MBEGU BORA YA KUKU WA KIENYEJI.
Kuku wa kienyeji wanaopatikana hapa nchini wamegawanyika katika makundi au Aina mbalimbali
Zifuatazo ni aina za kuku wa kienyeji wanaopatikana hapa nchini:
(i) Kuchi (Kuza), wana manyoya machache na wana maumbo makubwa.
(ii)Pono (Kishingo),
(iii) Njachama,
(iv) Kinyavu,
(v) Mbuni na
(vi) Tongwe (Msumbiji).
Kumbuka : Inashauriwa pia kufuga kuku wa kuchanganya damu (cross breed) yaani pandisha kuku wa kienyeji na wale wa kisasa (indigenous + Pure breeds) ili kuweza kupata kuku ambao kwa kiasi fulani huhimili magonjwa.
SIFA ZA MBEGU BORA ZA KUKU.
Kwa ajili ya ufugaji wa kuku wenye tija, chagua kuku wenye sifa zifuatazo:-
• Uwezo wa kutaga mayai mengi (kati ya 15-20) katika mzunguko mmoja wa utagaji.
• Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi.
• Uwezo wa kustahimili magonjwa.
• Anayetoka maeneo yasiyo na magonjwa; na
• Umbo kubwa na mwenye uwezo wa kukua haraka.
KUCHAGUA JOGOO BORA WA MBEGU.
Jogoo wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:
• Achaguliwe kutoka kwenye koo zenye sifa ya kutaga mayai mengi,
• Mrefu, umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu,
• Awe machachari, ushawishi kwa mitetea na ari ya kupanda; na
• Uwezo wa kupanda akiwa na umri wa miezi 7 – 10.
UCHAGUZI WA MAYAI.
Mayai kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
• Yaliyorutubishwa na jogoo,
• Yasiwe na nyufa,
• Yasiwe na maganda tepetepe,
• Yasiwe na kiini kilichovunjika,
• Yawe na ukubwa wa wastani; na
• Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2 baada ya kutagwa.
## 3. UTUNZAJI WA MAKUNDI MBALIMBALI YA KUKU.
utunzaji wa kuku hutegemea na Aina ya kuku mazingira, mfumo wa ufugaji unaotumika na umri wa kuku wenyewe.
UTUNZAJI WA MAYAI.
Mayai ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa kusimamishwa wima sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku 3 za mwanzo na kisha yageuzwe ili sehemu iliyo butu iangalie chini. Mayai yahifadhiwe kwenye sehemu iliyo na ubaridi kidogo na giza.
UTUNZAJI WA VIFARANGA
Malezi bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu vifaranga hawana uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara wanapoanguliwa. Ukosefu wa malezi bora husababisha vifaranga kuwa dhaifu, kufa kwa wingi na hivyo kupunguza idadi ya kuku wa baadaye. Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa kutumia kuku walezi au kutumia vifaa maalum.
KULEA VIFARANGA KWA KUTUMIA KUKU MLEZI.
Vifaranga wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku wengi wametotoa vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi aliye na uwezo wa kulea vifaranga wengi kati ya waliototoa aendelee kulea na wengine waliototoa waachwe huru ili warudi kwenye mzunguko wa kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga 20 hadi 25.
Mfugaji wa kuku, pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia yafuatayo:-
• Kuku anayelea vifaranga atengewe chumba maalum, apewe maji ya kutosha na chakula chenye virutubishi muhimu,
• Vifaranga wasiachiwe kutoka nje hadi watakapofika umri wa wiki 6,
• Vifaranga watengwe na mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama aendelee na mzunguko wa kutaga; na
• Katika maeneo yenye hali ya hewa ya ubaridi vifaranga wacheleweshwe kutenganishwa na mama/malezi hadi wiki ya 6 au mpaka waonekane wameota manyoya ya kutosha.
KULEA VIFARANGA KWA NJIA YA BRUDA.
Bruda ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwapatia joto vifaranga badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga wengi kwa kutumia bruda ambayo ni mduara unaoweza kutengenezwa kwa kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa kuziba pembe za chumba.
FAIDA YA KULEA VIFARANGA KWA KUTUMIA BRUDA.
1. Njia hii hupunguza vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na ndege au wanyama hatari,
2. Huruhusu kuku kutaga mapema zaidi na kuwa na mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). 3. Hurahisisha udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa kutumia bruda:-
• Kuweka vifaa vya kuongeza joto kwa mfano taa ya umeme, chemli au jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto katika bruda kinachohitajika. Wiki ya kwanza ni 35 C, wiki ya pili ni 33 C, wiki ya tatu ni 31 C na wiki ya nne ni 29 C,
• Kuchunguza mtawanyiko wa vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini hali ya joto. Wakijikusanya kwenye chanzo cha joto, inaashiria kuwa baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa mbali na chanzo cha joto maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
• Bruda iwe na sakafu yenye malalo yatokanayo na maranda ya mbao au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe endapo yataonekana yameloana,
• Bruda iwekwe vifaa vya maji na chakula. Maji na chakula kiwekwe kabla ya kuweka vifaranga,
• Vifaa vya joto viwekwe ndani ya bruda masaa 6 kabla ya kuingia vifaranga,
• Vifaranga walishwe chakula cha kuanzia gramu 12 - 15 kwa kipindi cha wiki ya kwanza na gram 15 - 21 kwa kipindi cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21 - 35 kwa kifaranga na chakula hicho kiwepo muda wote,
• Vifaranga wapatiwe vitamini, madini na dawa za kinga (antibiotics); na
• Vifaranga wapatiwe chanjo kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa mifugo. Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu Kama yatakavyoelezwa hapo mbele ni lazima.
UTUNZAJI WA KUKU WANAOFUGWA KATIKA MFUMO HURIA.
Kuku wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora yakiwemo yafuatayo;
• Wapewe chakula cha ziada asubuhi kabla ya kutoka na wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza kugawanywa mara 2 kwa siku,
• Wapatiwe maji safi na ya kutosha wakati wote; na
• Wapatiwe chanjo na dawa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
UTUNZAJI WA KUKU WANAOFUGWA KATIKA MFUMO WA SHADIDI.
• Majogoo watenganishwe na mitetea katika wiki 7 hadi 10 ili kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
• Wapewe chakula cha kukuzia kuanzia wiki ya 8 - 15 gramu 55 - 60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65 - 80 kwa wanaofugwa mfumo huria na gram 120- 125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa mfumo wa shadidi,
• Kuku wa nyama wapatiwe chakula cha kuku wa nyama muda wote,
• Wapatiwe maji safi ya kunywa kwa muda wote kwenye vyombo visafi,
• Kuku wachunguzwe dalili zozote za ugonjwa ili waweze kupata tiba sahihi kutoka kwa mtaalamu wa mifugo,
• Kuku wa wiki 9 - 20 wanahitaji nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa kuku,
• Kuwe na vyombo maalum vya kutosha kwa ajili ya chakula na maji
• Wafanyiwe usafi wa banda mara kwa mara ili kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu; na
• Wakatwe midomo ili kuzuia kudonoana.
UTUNZAJI WA KUKU WANAOTAGA.
Mahitaji ya kuku wanaotaga ni tofauti na ya makundi mengine. Mambo ya kuzingatia kwa kuku wanaotaga ni pamoja na:-
• Banda liwe na viota vya kutagia mayai (kiota 1 kwa kuku 3 - 5). Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha umri wa wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
• Wapatiwe chakula na maji safi wakati wote kwa kutumia vyombo maalum ambavyo ni visafi,
• Kuku wasiotaga waondolewe kwenye kundi. Kuku hao huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na kavu, upanga wake kichwani (comb) huwa mdogo na mwekundu,
• Wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3,
• Wawekewe fito au ubao mwembamba kama sehemu ya kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
• Mayai yakusanywe mara 4 au zaidi kwa siku ili yasidonolewe na kuku,
• Kuwe na malalo makavu na yabadilishwe mara yanapochafuka,
• Vyombo vifanyiwe usafi kila siku ili kuzuia magonjwa; na
• Watundikiwe majani mabichi aina ya mchicha, papai, alfaalfa, majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe
LISHE YA KUKU:
Ili kuku waweze kuishi, kukua vizuri, kunenepa na kutaga mayai mengi ni lazima wale chakula kingi na chenye ubora unaotakiwa. Uwingi na ubora wa
lishe ya kuku unaweza kuainishwa katika makundi ya vyakula kama ifuatavyo:
1. Vyakula vya kutia nguvu
2. Vyakula vya kujenga mwili
3. Vyakula vya kuimarisha mifupa
4. Vyakula vya kulinda mwili
5. Maji.
1. VYAKULA VYA KUTIA NGUVU
Vyakula vya mifugo vifuatavyo vinawekwa katika kundi hili;
a. Pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano.
b. Nafaka kama vile mtama , chenga za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi
c. Mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi. Kabla ya kulisha kuku hakikisha mizizi hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili imo katika vyakula vya aina hii. Inashauriwa kuwa mizizi hiyo ilishwe kwa kiasi cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.
Katika kundi hili la kutia nguvu ,pia yakula vya mafuta kama vile mafuta ya kutoka kwenye vyakula vya mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kutia nishati huchangia asilimia 60-70 ya mchanganyiko wote wa chakula.
2.VYAKULA VYA KUJENGA MWILI.
**Mashudu :Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula v vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya ,korosho, na ufuta .
**Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), hii inafanywa ili kuepusha uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukiza .
**Mabaki ya samaki ya samaki/dagaa na nyama.
**Vyakula asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, Masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.
***Vyakula hivi huchangia asilimia 20 hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.
3. VYAKULA VYA KUIMARISHA MIFUPA (Madini)
(a)Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kuuweka mwili wa ndege (kuku) katika hali ya afya njema kwa ujumla.
(b) Madini ya muhimu ni madini ya chokaa (
calcium) na fosiforasi (phosphorus). Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa maganda ya konokono na mayai yaliyosagwa vizuri. Lakini inapendekezwa kwamba unapoongeza madini ya fosforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyopasa ,kwasababu kiwango cha aina moja kikizidi kuliko cha aina nyingine husababisha upungufu wa kile kidogo
Viinilishe vya madini vinavyotakiwa ni pamoja na;
:Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa . Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vijidudu vya maradhi.
:Chumvi ya jikoni
:Madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate
:Magadi (kilambo).
4. VYAKULA VYA KULINDA MWILI.
Vyakula katika kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;
**Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, Chinese kabeji n.k.
**Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).
** Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamini A na D zinatumika vizuri mwilini, kwahiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao unaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.
***Chakula cha kuku wanaofugwa ndani ni lazima kichanganywe na vitamini zinazotayarishwa viwandani.
MCHANGANUO WA VIINILISHE VYA CHAKULA CHA KUKU:
i. Vyakula vya kutia nguvu mwilini:
:Pumba za mahindi
kilo 48
:Pumba laini za mpunga
kilo 26
JUMLA KILO 74.
ii. Vyakula cha kujenga mwili
:Mashudu ya alzeti kilo 18
:Damu ya wanyama kilo 1
:Mabaki ya samaki /dagaa kilo 3
JUMLA KILO 22.
iii.Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini):
1. chumvi ya jikoni
kilo ½
2. chokaa(dicalciumphosphate)…
kilo 2
3. poultry premix/
kilo ½
4. unga wa mifupa kilo 1
JUMLA KILO 4
MUHTASARI WA MAHITAJI YA VIINI LISHE:
***Vyakula kutia nguvu mwilini
kilo 74
***Vyakula vya kujenga mwili
kilo 22
***Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini) kilo 4
JUMLA
100
Jumla ya mchanganyiko wa vyakula
kilo 100
CHAKULA CHA NYONGEZA.
Ili kuhakikisha kwamba kuku wanapata viinilishe vya kutosha kuku wanaweza kupewa mchwa na mafunza.
Vilevile vitu mbadala aina ya nafaka vinavyopatikana hutegemea sana aina ya mazao yanayolimwa katika eneo husika.
MBINU ZA KUOTESHA FUNZA KWA AJILI YA CHAKULA CHA KUKU.
Funza na mchwa ni chakula kizuri na rahisi chenye viinilishe aina ya protini kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo huria unaoboreshwa. Hata hivyo vyanzo hivi vya chakula cha protini huchangia tu vile ambavyo kuku wanatakiwa kupewa.
a. Inashauriwa uwape vifaranga hao funza na mchwa kwa sababu ndio wanaohitaji protini kwa kiasi kikubwa na cha kuaminika.
Funza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa njia rahisi na kutumika kuboresha chakula cha vifaranga.
c) Mafunza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa kutumia damu, viungo vya ndani ya tumbo la ng’ombe pamoja na samadi ya ng’ombe.
d) Chungu kijazwe maji theluthi moja ya ujazo wake, inzi watakuja na kutaga mayai katika mchanganyiko ambao mafunza walioteshwa wataanza kula mchanganyiko huo.
e) Baada ya hapo vitu hivi vyote vitachanganywa pamoja katika chungu kimoja kikubwa ambacho kitaachwa wazi wakati wa mchana na kufunikwa wakati wa usiku.
f) Siku tano baadaye maji yatajazwa kwenye mtungi huo na mafunza yatakusanywa wakiwa wanaelea juu. Baada ya kukusanya waoshe vizuri na maji halafu lisha kuku moja kwa moja.
g) Kumbuka kuweka chungu kinachooteshwa mafunza kuweka mbali na maeneo ya watu ili kuepuka harufu inayoweza kusumbua watu.
KWA UFUPI
=/ Ni vigumu kukadiria mahitaji ya chakula cha kuku wanaojitafutia chakula, lakini inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani lakini wale kuku wanafugwa kwa mfumo wa huria nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .
=/ Hakikisha kuku wanawekewa chakula na maji safi kwenye vyombo safi na kubadilisha kila vitakapoisha.
## 4. UDHIBITI NA TIBA DHIDI YA MAGONJWA.
Kuku wanaopata lishe bora,
kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yanayotokea mara kwa mara huwa na afya nzuri. Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama. Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba.
MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUZUI MAGONJWA KWA KUKU.
• Banda liwe safi muda wote,
• Kabla ya kuweka kuku, banda linyunyiziwe dawa ya kuua wadudu wa magonjwa mbalimbali,
• Kuku wakaguliwe kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
• Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,
• Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
• Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,
• Banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine,
• Lango la kuingilia katika banda la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea vya wadudu wa magonjwa; na
• Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote.
DALILI ZA MAGONJWA
Dalili za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama zifuatazo:-
• Kuzubaa,
• Kupoteza hamu ya kula,
• Kujitenga na wenzake katika kundi; na
• Kupunguza au kusimama kutaga.
Mfugaji anapoona mojawapo ya dalili hizo amwone mtaalam wa mifugo
MAGONJWA YANAYOSABABISHWA NA VIRUSI
1. Mdondo (Newcastle):
Dalili zake:
kuku kukohoa,kuhema kwa shida,kutokwa na ute mdomoni na puani,hupatwa na kizunguzungu, kuharisha mharo wa kijani na manjano na hatimaye kuku hufa ghafla. Vifo huweza kufikia asilimia90
2. NDUI YA KUKU: Fowlpox)
Kuku hupatwa na vipele vya mviringo kwenye upanga, (masikio,miguu na sehemu zisizo na manyoya.vifo vichache kwa kuku wakubwa, wadogo huweza kufa nusu ya kundi.CHANJO WIKI YA NANE
(wapewe antibiotic na vitamini) hakuna tiba)
3. MAHEPE (.Marek’s disease)
Kuku kupooza miguu, mabawa na shingo huweza kupinda, mara nyingi huwapata kuku wenye umri wa wiki ya 16 hadi 30.kiasi cha robo ya mitemba wanaweza kufa.
(chanja vifaranga wakiwa na umri wa siku moja)
4. GUMBORO :
vifaranga huharisha mharo mweupe,huhangaikahangaika, hushindwa kuhema, manyoya husimama, hudumaa, hutetemeka na hatimaye hufa.vifo vyaweza kufikia 5% hadi 10%.
(Hakuna tiba wapatiwe chanjo ya gumburo)
5. MAGONJWA YASHAMBULIAYO MFUMO WA HEWA
(Infectious bronchitis, laryngotracheitis or chicken influenza)
upungufu wa mayai kwa kuku wanaotaga,vifaranga hupata matatizo ya kupumua na kupiga chafya na hufa kwa wingi
(huzuiwa kwa chanjo) hakuna tiba).
6. MAFUA MAKALI YA NDEGE:
kupumua kwa shida, kukohoa na kupiga chafya, sehemu za kikole(kidevu na kishungi) hubadilika na kuwa rangi ya zambarau,kutokwa na machozi,kupinda shingo na kuanza kuzunguka, kuvimba kichwa, kuharisha kinyesi chenye majimaji, rangi ya kijani na baadaye kinyesi cheupe.
7. HOMA YA MATUMBO: (Salmonella gallinarum)
ugonjwa huu unaweza kurithiwa kupitia kwenye mayai au kuambukizwa kutokana na kuku wagonjwa, kinyesi, kudonoana, na mazingira machafu,
Kuku huharisha mharo wa kijani, vilemba na upanga hupauka kutokana na upungufu wa damu, manyoya husimama.vifo huweza kufikia 50%.
Weka banda katika hali ya usafi,ondoa kuku waliougua,usitumie mayai yenye ugonjwa kuangulia.
8. Pullorum bacillary white diarrhea (bacteria salmonella pullorum)
huathiri zaidi vifaranga(kabla ya umri wa wiki 4) vifaranga hujikusanya pamoja na kutetemeka kama waliopatwa na baridi.huharisha mharo mweupe hamu ya kula hupungua,manyoa hunyea na hupumua kwa taabu na vifo huweza kufikia hadi asilimia 50.
9. kipindupindu cha kuku(Fowl cholera)
kuku kuhara mharo wa rangi ya njano.
Husinzia na kulegea,
Hulala kichwa kikining’inia kwenye mabawa.
Manyoya husimama,
kuhema kwa shida,
Hushindwa kusimama na hatimaye hufa na vifo huweza kufikia asilimia 50
##: Usafi wa banda(huweza kutibika kwa dawa ya sulfa)
10.Ugonjwa unaoshambulia mfumo wa hewa (chronic respiratory)
Kuku kupata mafua, kukohoa kushindwa kupumua, kutokwa na makamasi,vifaranga hudumaa,utagaji hupungua na viungo vya mifupa huweza kuvimba
Tiba: antibiotic hutibu,usafi wa banda.
11. UGONJWA WA KUHARA DAMU:
Kuku huharisha kinyesi kilichochanganyika na damu na mara nyingine damu tupu,hudhoofisha kuku, huteremsha mabawa na hatimaye kuku huweza kufa.
Usafi wa banda,hutibiwa kwa kutumia dawa kama vile Amprolium.salfa na Esb3. Pia muone daktari wa mifugo kwa ushauri zaidi.
DAWA ZA KIENYEJI KWA KUKU.
(1). ugonjwa wa KIDERI (Newcastle desease).
Hapa mimea mikuu mitatu hutumika sana ambayo ni ALOE VERA, KATANI , MWAROBAINI
(I) Chukua KATANI MBICHI(ie ya kijani ambayo haijakauka) unatwanga kwenye kinu, maji au ule uji uji wake unaukusanya, unaweka kwenye vyombo safi na unaongeza maji kiasi ili kupata mchanganyiko mzuri, Kwa kuwa ni dawa ya kienyeji haina kipimo maalumu sana, ila unatakiwa ukadirie isiwe kali sana wala isiwe nyepesi sana, cha msingi lile povu povu lake lisipotee, dawa hii ni kinga nzuri sana kwa KIDERI(New Castle). Wape kuku kwenye maji yao ya kunywa angalau kila mwezi SIKU TATU au SIKU NNE mfululizo na ni kwa umri wowote ila wasiwe vifaranga wadogo sana.
(ii) ALOEVERA (shubiri) , chukua aloe vera twanga na changanya na maji kidogo ili isiwe kali sana na pia zingatia isiwe nyepesi sana kisha wape hiyo juisi kama maji ya kunywa. Baada ya hapo unakaa kama wiki mbili au tatu unawapa MUAROBAINI. Lakini hii ni kinga tu sio tiba na haina madhara, ila wakiumwa inabidi ufuata ushauri wa daktari wa mifugo.
2. KUHARA
Kama kuku wako wanaonesha wana ugonjwa wa kuhara na ukajaribu dawa za Madukani na zikashindwa kufua dafu, au wanahara na hujui ni ugonjwa gani kwani kuhara kunaambatana na magojwa chungu nzima, basi dawa hapa ni MAJANI YA MPERA.
Twanga majani ya MPERA AMBAYO HAYAJAKAUKA na ile juisi yake wawekee kwenye maji, ila kama unataka ifanye kazi vizuri changanya na MUAROBAINI na ALOE VERA, kuku wako watafunga kuhara mara moja na haina madhara yoyote kwani kuku hupenda sana kula majani. Unaweza kuwapa siku nyingi kadiri utakavyo ila ni vizuri ikawa siku tano mfululizo kwa mwezi mmoja.
KUMBUKA : ni vizuri ukiwa umepanda ALOE VERA, MUAROBAINI na KATANI maana ni muhimu Sana na hutibu magonjwa mengi Sana sio kwa kuku tu Bali hata kwa binadamu pia.
## 5. UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU.
Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ndege wengine wafugwao ili kusaidia mfugaji kujua maendeleo ya ufugaji wake. Utaratibu wa kuweka kumbukumbu mara tukio linapotokea ni lazima ili kuepuka kusahau. Mfugaji ahakikishe anaweka kumbukumbu ambazo ni sahihi na zinazoeleweka.
AINA ZA KUMBUKUMBU.
Kumbukumbu zinazopaswa kuwekwa ni pamoja na:-
• Aina na idadi ya kuku waliopo kwenye kila kundi (mfano vifaranga, wanaokua, wanaotaga, majogoo),
• Uzalishaji wa mayai kwa kundi la kuku waliopo,
• Utotoaji wa vifaranga,
• Kinga na matibabu,
• Mapato na matumizi,
• Utagaji wa kila kuku na utunzaji (kwa kuku wa asili); na
• Kumbukumbu za vifo.
ZINGATIA: Kumbukumbu ni kipimo cha mafanikio ya kazi yako unayoifanya. Inakusaidia kujua mapato na matumizi kwa ufasaha.
Bila kutunza kumbukumbu huwezi kujua maendeleo yako.
"Mali bila daftari huisha bila ya taarifa ".
NIMEJARIBU KUELEZA VITU VINGI AMBAVYO NI MUHIMU KUHUSU UFUGAJI WA KIENYEJI.
Pia maarifa zaidi kuhusu ufugaji yanapatikana katika Vitabu mbalimbali, hivyo ni muhimu Sana kujisomea Vitabu ili kujiongezea maarifa zaidi.
Motto: "Internal power can change the world".
Pia kwa Masada tunaweza kuwasiliana.
+255764075392
Email : lucastrngwakwa@gmail.com
Endelea kutembelea blog yako uipendayo http://ngwakwaufanisi.blogspot.com
Unaweza kuacha email yako hapo chini uwe unapata makala kila zinapochapwa.
Ahsante.
