Ticker

6/recent/ticker-posts

UKWELI USIOPINGIKA
SEHEMU YA 6: KUONGEZA THAMANI
Thamani Ni ubora wa kitu unaotokana na hali yake umuhimu wake, Ni bei au gharama ya kitu. Ni UKWELI USIOPINGIKA kuwa Mafanikio ya MTU yoyote yamejificha ndani ya thamani. Ukitambua thamani yako Ni lazima utatafuta thamani ya maisha yanayoendana na maisha unayotaka kuishi kulingana na thamani yako.  Ni ukweli usiopingika kuwa kutambua thamani hukufanya uwe na juhudi katika kuitafuta thamani hiyo. Thamani unazoweza kuzitafuta zinaweza kugawanyika katika makundi makuu matatu:
> Thamani yako binafsi.
> Thamani kwa watu wengine
> Thamani ya Huduma au bidhaa.

1)Thamani ya mtu binafsi.
Thamani ya MTU binafsi ni vitu vile ambavyo unaamini ni vya muhimu zaidi katika maisha yako na katika kazi yako.
Ni UKWELI USIOPINGIKA kuwa kila MTU alizaliwa na thamani inayoitwa utu na thamani hiyo (utu) unaweza kukua au kufifia kwa kadri kadri mtu anavyoendelea kuutumia, kuishi na kadri umri unavyoongezeka.
Utu au thamani ya MTU binafsi inaweza kukuzwa ama kuhafifishwa na vitu vikuu vinn.
Moja, utu au thamani katika mavazi. Ni ukweli usiopingika kuwa mavazi yana mchango mkubwa sana katika kuhafifisha au kukuza thamani ya MTU. Kwa kadri utakavyovyaa ndivyo mavazi ya Heshima au kustiri mwili ndivyo thamani yako itakavyositawi zaidi na kushindwa kuvaa mavazi yenye heshima ndivyo utu wako na thamani yako itakavyoshuka. Kuna msemo mmoja usemao "Vaa kama vile wewe ndio mmiliki wa Benki, usivae kama unataka kuomba mkopo benki"
Pili, Utu au thamani katika Vyakula. Kwa kadri utakavyojithamini wewe binafsi bila shaka utathamini chakula unachokula, kwa sababu chakula unachokula ndicho huleta thamani ya mwili wako, akili yako na hata roho yako pia. Ongeza thamani kwenye chakula chako lakini usimsahau yule ambaye hana uwezo wa kupata chakula kama unachokula.
Tatu, Thamani katika elimu. Thamani ya elimu ninayoiongelea hapa Ni aina zote za elimu (Elimu rasmi na elimu siyo rasmi) kwa ujumla hapa naongelea maarifa na ujuzi. Ni lazima uongeze thamani ya Elimu yako kwa kusoma shuleni kwa bidii, kujisomea vitabu na majarida yatakayokuongezea maarifa. Ni UKWELI USIOPINGIKA KUWA katika ulimwengu wa sasa MTU mwenye elimu au mwenye kitu kichwani au mfukoni ndiye huonekana ana thamani. Kuongeza thamani ya Elimu yako siyo lazima uingie shule, jibidishe kutafuta maarifa popote pale unapoweza kuyapata.
Nne, Thamani kwenye burudani. Burudani ina umuhimu Mkubwa sana katika kuongeza thamani ya utu wako. Burudani nzuri huitibu nafsi yako na kukufanya uone thamani kubwa ilipo ndani yako, lakini burudani mbaya huharibu akili na kupunguza uwezo wa kufikiri sawasawa. Chagua burudani unayofanya, unayotazama au kusikiliza hiki kitaongeza thamani yako binafsi. Mwandishi mmoja aliyevuviwa aliandika "By beholding we become changed" ikimaanisha "kwa kutazama tunabadilishwa".
>Thamani ina mchango Mkubwa sana katika tabia, mtazamo, na hali ya MTU na ni Mwongozo muhimu na mpana sana katika hali zote.

2). Thamani ya watu wengine.
Ni muhimu sana kutambua thamani ya watu wengine katika mafanikio yako, thamani yako inatokana na namna watu wengine wanavyokuthamini kama hutambui thamani ya watu wengine pia wao hawatatambua thamani yako hivyo utakuwa huna thamani (thamani itashuka).
Thamani kwa watu wengine inaweza kuchangiwa na maeneo yafuatayo:
Moja, Utu katika uongozi au siasa. Siasa au uongozi unaweza kukuza thamani ya watu wengine au kuhafifisha thamani ya watu wengine. Kiongozi bora ni yule anayetambua thamani ya watu anaowaongoza, anajilinda ili aendane nao na kuwainua ili kufikia thamani anayotaka wawe nayo hata kama hawakuwa nayo. Ongeza thamani ya wale unaowaongoza na wale wanaokuongoza ili thamani yako iongezeke pia.
Pili, utu au thamani kwenye familia. Ni ukweli usiopingika kuwa MTU mwenye familia yenye heshima na mtu anayetoka katika familia Inayoheshimika huwa anaheshimika na kuthaminiwa pia. Jifunze kuwathamini watu wa nyumbani mwako, usiwadharau au kuwakosoa kila Mara hata kama unawazidi kila kitu. Thamani uliyonayo na unayoweza kuipata kwa sehemu kubwa huchangiwa na familia yako (Baba, mama, kaka, Dada n.k ).
Tatu, Thamani ya marafiki. Uthamani wa marafiki ndio uthamani wa maisha yako. Chagua marafiki ambao wana thamani kwako ili maisha yako yawe na thamani. Kuna msemo usemao "nioneshe marafiki zako nami nitakuambia tabia yako" Hivyo basi jitahidi kuongeza thamani ya marafiki zako ili uongeze thamani ya maisha yako na ukuaji wa mafanikio yako.

3). Thamani ya huduma au bidhaa.
Kuongeza thamani ya bidhaa au huduma ni njia ya kawaida ya kubadilishaba au kuchakata mazao au bidhaa kabla ya kuiweka au kuiingiza sokoni kutoka katika hali yake ya kawaida.
Ili kuongeza thamani ya bidhaa au huduma yako ni lazima uwe na juhudi na ubunifu katika kazi. Kazi ndio kipimo cha thamani au utu wa mtu. Ni UKWELI USIOPINGIKA kuwa watu wengi wanaofanikiwa zaidi kiuchumi ni wale walio na uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa au Huduma kutoka katika hali ya kawaida.

>Kabla ya kuongeza thamani ya mazao katika kilimo zingatia vitu vifuatavyo:
1. Mazingira ya kuzalishia.
Kwa mkulima mazingira yake ya kuzalishia ni shamba. Mazingira hayo lazima yaboreshwe kwa kutiliwa mbolea kusafishwa na kuondoa kila kikwazo kitakachopunguza ubora wa mazao.

2. Dhibiti magonjwa dhidi ya mimea.
Bila shaka mimea ambayo haina kinga dhidi ya magonjwa mazao yake pia yatakuwa hafifu na yenye thamani ya chini sana. Hivyo basi kama unahitaji kufanikiwa katika kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao tumia juhudi zako zote kuthibiti wadudu, magonjwa na wanyama waharibifu kwa mimea.

3) Uhifadhi bora au vifungashio.
Baada ya mazao yako kukomaa namna utakavyoyahifadhi ndicho kitu kitakachochangia thamani yake pindi kitakapokuwa sokoni.
Mfano: MTU aliyevuna matunda na kutengeneza juisi safi kisha kuihifadhi katika vifungashio vizuri, mtu huyu atakuwa ameongeza thamani ya mazao yake maradufu.

NAMNA YA KUTAMBUA THAMANI YAKO.
Ni muhimu sana kutambua thamani yako kwa sababu thamani husimama kama kama mwongozo kwenye matukio unayokumbana nayo katika maisha. Kama ilivyo muhimu kujitambua kama nilivyoeleza katika SEHEMU YA 4: KUJITAMBUA ya mwendelezo huu kadhalika pia ni muhimu baada ya kujitambua ukaanza Mara moja kuongeza thamani yako.

KUSOMA SEHEMU YA NNE BOFYA
https://ngwakwaufanisi.blogspot.co.ke/2017/04/ukweli-usiopingika-sehemu-ya-4.html?m=1

Zifuatazo ni hatua tano za kuongeza thamani yako:
1. Tafuta upekee wako.
Ni UKWELI usiopingika kuwa kila mtu ni wa pekee na hafanani na mtu mwingine kwa kila kitu. Jiulize wewe ni wa pekee kiasi gani? Kwa namna gani unatofautiana na mwingine? Tumia upekee huo kutambua thamani yako. Upekee wako huo una thamani gani kwako, kwa wengine na kwenye mafanikio yako?

2. Pima maisha yaliyopita (background).
Fikiria historia ya familia unayotokea, ni vitu yani vya muhimu ambavyo ni vya thamani walivyokuwa navyo wazazi wako na namna gani inafanya ili kuviendeleza?
Je kuna vitu gani vya thamani unavyoweza kuvifanya sasa na Fikiria ni kitu gani utakachokiacha baada kwa watoto wako baada wewe kupita?

3.Tambua nguvu yako ya Ushawishi na mchango wako.
Angalia namna ambavyo wanakuona, ni muhimu kumuuliza mtu unayemwamini juu ya namna anavyokuona, Namna wengine wanavyokuona na namna watu wanavyosema kuhusu wewe. Kama kuna mabaya yanayosemwa kuhusu wewe yaache Mara moja.
Pia jiulize ni thamani gani uliyo nayo inayopelekea wengine wafanye hivyo wanavyofanya kwako?.

4). Tambua chaguzi zako.
Ni muhimu sana ukatambua namna unavyofanya uchaguzi, thamani ya uchaguzi unaofanya na matokeo yake.
Chagua marafiki zako wa karibu walio na mtazamo chanya ili waweze kuongeza thamani ya maisha yako.
Jiulize, huwa unaonesha mwitikio gani pale unapokuwa kwenye magumu? Ni namna gani unafanya maamuzi katika wakati kama huo.

5.Kuwa mtu wa kuihoji. Kujihoji hukufanya uwe mtu wa thamani zaidi kwa sababu kila kitu utakachokuwa unakifanya utakuwa ushakifanya kwanza katika mawazo yako. Ni UKWELI usiopingika kuwa watu wengi waliofanikiwa ni watu wa kujihoji sana, kwa nini nifanye hivi na nisifanye vile.

Mpendwa msomaji bila shaka tutakuwa tumeangalia mengi sana kuhusu kuongeza thamani ya mtu binafsi, thamani ya watu wengine na thamani ya bidhaa na Huduma.
Pia tumeangalia namna ya kutambua thamani yako, hivyo ni wajibu wako kubaki hivyo ulivyo au kufanya Yale yatakayoongeza thamani yako.

Tukutane katika sehemu ya mwisho ya mwendelezo huu wa UKWELI usiopingika.

LUCAS ROBERT
+255764075392
+255713056903
lucastrngwakwa@gmail.com

"Live an inspired Life"