Ticker

6/recent/ticker-posts

TAA SABA ZA MJASIRIAMALI. SEHEM YA KWANZA

TAA 7 ZA MJASIRIAMALI.
SEHEMU YA 1: UTANGULIZI.
NI Wazi kuwa Neno MJASIRIAMAKI limejichukulia umaarufu Mkubwa sana katika siku za hivi karibuni kwa kukaa sana katika akili za watu na kutamkwa sana katika midomo ya watu. Pamoja na kwamba neno hili tunalitumia Mara kwa Mara katika mazungumzo yetu ya kila siku ni dhahili kwamba kuna uwezekano Mkubwa kuwa wengi wetu tumekuwa tukilitumia bila kufahamu hata maana yake.

Hebu tuangalie asili na maana ya MJASIRIAMALI NA UJASIRIAMALI.
>>Neno mjasiriamali lina asili ya neno la kifaransa "entreprendre" likimaanisha kufanya Kazi kwa kujitegemea ama kufanya Kazi katika uwanja wako binafsi na kwa tafsiri fupi ni KUJIAJIRI.

>>Mjasiriamali ni mtu ambaye yupo tayari kuthubutu au kuanzisha jambo jipya ambalo litampa faida au litakuwa na nafasi ya kumpa faida hapo daadaye. Lakini wengine wanadai kuwa mjasiriamali ni
mbunifu ambaye anaunadi ubunifu wake na kuutumia ili apate faida. Wengine wanasema "mjasiriamali anabuni bidhaa mpya au njia mpya ya uzalishaji wa bidhaa ambayo soka linahitaji bidhaa hiyo au hiduma hiyo ambayo haijapata kusambazwa hapo kabla".


>>Mnamo karne ya 20 mwanauchumi Joseph compete (1883-1950) anamtazama mjasiriamali kama "mvumbuzi (innovetor) , mbunifu ,anayeleta mageuzi na mabadiliko katika solo au biashara". Mchanganyiko mpya wa ubunifu na msukumo alionao mjasiriamali ndio unaotoa nafasi au kusaidia viwanda vya zamani kubadilika na kuwa na mfumo mpya wa kuzalisha , kufanya biashara na kutoa huduma.

Mtaalamu wa biashara Peter Drunker anaendeleza wazo hili kwa kusema kuwa "mjasiriamali ni mtu ambaye amejikita katika kufanya utafiti kwa lengo la kuleta mabadiliko na anawajibika katika mabadiliko hayo.

>> Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa ujasiriamali ni kitendo cha kufanya uamuzi wa kuanzisha kitu kipya au biashara mpya, au kufanya jambo ambalo linafanywa na wengine lakini katika njia tofauti huku ubunifu na mipango thabiti inayoambatana na ujasiri vikiwa ndiyo nguzo kuu kwa ushirikiano na msukumo wa dhati wa kufanya kazi kwa bidii.


> Je kuna tofauti yoyote kati ya mjasiriamali na mfanyabiadhara?

Katika nchi ya Tanzania matumizi ya neno mjasiriamali yameangezeka sana katika miaka ya hivi karibuni (miaka ya 2000).
Wengi wetu tumekuwa tukichanganya sana matumizi ya haya maneno mawili (mjasiriamali na mfanyabiashara),  Unaweza kukuta mtu anajiita mjasiriamali kumbe ni mfanyabiashara. UKWELI ni huu "mjasiramali ni mfanyabiashara lakini si kila mfanyabiashara ni mjasiriamali".

Hebu tupitie namna ambavyo wataalamu mbalimbali katika masuala ya uchumu walivyojaribu kuyatofautisha haya maneno. Katika miaka ya 1800, mchumi wa kifaransa , J.B Say alisema "ujasiliamali ni kitendo cha kubadilisha rasilimali za kiuchumi kutoka kwenye kiwango cha chini cha uzalishaji na kwenda kwenye kiwango cha juu cha uzalishaji". Wasomi wengine wa Kiingereza Stokes, Wilsons na Mador wao walisema ujasiliamali unahusisha kitendo cha kuongeza thamani kutokana uvumbuzi kwenye masoko ya kibiashara.
 Hapa neno uvumbuzi linamanisha kuleta kitu kipya kwenye soko la kibiashara.

Vipo vigezo au sifa NNE (4) zinazowatofautisha mjasiriamali na mfanyabiashara. Nazo ni kama ifuatavyo:-
1: Kiwango cha faida/thamani  kinachotengenezwa.
 Lengo la mjasilimali kujiingiza kwenye biashara si kutengeneza kiasi ambacho kinakidhi mahitaji yake ya kila siku tu., La hasha!  Lengo kuu ni kuweza kutengeneza mamilioni mengi ya pesa ili kuridhisha msukumo unaotoka ndani ya mwili wake. Kwa maana hii ndiyo maana mjasiliamali wanakuwa na tabia tofauti sana na mmiliki/mfanya biashara wa kawaida.

2: Muda wa Kutengeneza hiyo faida.
Mfanya biashara huwa hategemei sana faida ya haraka kama mjasiliamali. Pia kwa mjasiliamali ikiwezekana anaweza hata kuiuza biashara yake kwenye kipindi kifupi tangu kuanzishwa kama ana uhakika wa kutengeneza mamilioni ya shilingi kwenye mauzo. Mjasiriamali hupenda sana mzunguko wa pesa wa haraka na hucheza sana na mazingira. Hutumia muda mwingi kuangalia ni Fursa gani ambayo inaingiza pesa nyingi kwa sasa.

3: Mjasiliamali hufanya biashara kwenye mazingira hatarishi (Risk taker) zaidi kwa kutegemea faida kubwa.
Hivyo bila hiyo shauku ya ujasiliamali isingekuwepo kwa sababu nani angekuwa yuko tayari kujiweka kwenye mazingira makubwa hatarishi kwa kupata faida au thamani ndogo. Kutokana na fauda kubwa ambayo mjasiriamali huiona endapo atafanikiwa ndicho kitu ambacho humvutia kujiingiza katika hizo biashara zenye changamoto, ngumu na zenye hatari nyingi.

4:Uvumbuzi (Creativity):
Ni jambo ambalo linahusiana kwa kiasi kikubwa na ujasiliamali, uvumbuzi ndio  na unaoipa biashara ya mjasiliamali faida za kiushindani ambayo ndiyo inayotengeneza utajiri au mamilioni mengi ya pesa. Uvumbuzi huu unaweza kuwa kwenye bidhaa, soko, huduma au mchakato mzima wa uendeshaji wa biashara.
UTAJIRI unapatikana pindi UGUNDUZI unapoenda sambamba na MAHITAJI, kwa mtazamo huu tunaweza kusema ya kwamba kazi ya Mjasiriamali ni sawa na kuunganisha mbegu za vigezo fulani katika hali ya Ugunduzi na Ubunifu ili kutengeneza ubora na thamani kwa mteja kwa imani ya kwamba thamani itakayopatikana itafidia gharama za mbegu hizo, na hatimaye kutengeneza faida ya kutosha inayopelekea UTAJIRI.

MAMBO UNAYOTAKIWA KUFANYA KABLA YA KUWA MJASIRIAMALI.
Kutokana na faida kubwa inayoonekana kwenye ujasiriamali wengi wetu huamua kujiingiza katika ujasiriamali kabla ya wakati. Naweza kuuita kwa lugha ya kiingereza "pre mature entrepreneurship" Kwa sababu unaingia bila hata kumfahamu mjasiriamali ni nani na anatakiwa awe na sifa gani.
> Ikiwa utaingia katika ujasiriamali bila kujua ni nini cha kufanya unaweza usitamani kuingia tena na pengine ukauchukia ujasiriamali milele, na kitendo cha kuchukia ujasiriamali tu ndiyo chanzo cha umaskini.
>>Hivyo basi kabla hujajiingiza katika ujasiriamali Fanya yafuatayo:-

1. KUWA MVUMILIVU NA JIFUNZE KUJIPA MOYO
Maisha ya ujasiriamali sio ya mtelemko Wala lelemama. Unaweza kukutana na changamoto mbalimbali ukiwa unaelekea mafanikio. Wengi hukata tamaa njiani kwa sababu ya hili. Wale wasiokata tamaa ni wale wenye uwezo wa kujisukuma kusonga mbele hata kama kila kitu kinaenda vibaya. Ni uwezo wa kujipa tumaini la mafanikio hata kama hujaambulia kitu siku hiyo katika biashara yako. Ni uwezo wa kuinuka baada ya kuanguka mara kadhaa. Ni uwezo wa kujivuta na kusogea mbele hatua moja zaidi hata kama unajihisi kushindwa kabisa. Hivyo kabla ya kuwa mjasiriamali ni lazima ujifunze kuvumilia maumivu kama hayo.

2. JIFUNZE KUWEKA AKIBA
Wengi wetu tunaufahamu vizuri methali isemayo "Haba na haba hujaza kibaba" Methali hii inaeleza vizuri kabisa umuhimu wa kuchuma kidogo kidogo na kuweka akiba. Wengi wetu tunajiuliza maswali mengi sana jinsi ya kupata mtaji ili kuanzisha biashara. Ukitazama wafanyabiashara wengi wakubwa leo walianza na mitaji waliyoipata baada ya kutunza pesa za mishahara au biashara nyingine ndogondogo. Ikiwa hutafanya hivyo sahau kitu kinachoitwa ujasiriamali kwako. Kuwa na kiasi kizuri cha pesa cha akiba kunaweza kuokoa biashara yako wakati wa misukosuko.

3. JIFUNZE MBINU ZA KUTOA HUDUMA / MBINU ZA MAUZO.
Ukitaka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio ni lazima ujifunze nmna ya kuhudumia watu. Kuanzia kujua jinsi ya kupokea wateja hadi jinsi ya kuagana nao wakishanunua bidhaa kutoka kwako, mbinu za mauzo hutumika. Hili ni jambo ambalo inabidi uanze kulielewa mapema kama unataka kuwa mjasiriamali. Unaweza kuanza kidogokidogo kwa kuongea na watu walio wajasiriamali, kujisomea vitabu na machapusho mbalimbali au kwa kufanya uchunguzi mtaani kwako.

4. TENGENEZA UHUSIANO MZURI NA WATU WENGINE.
NI wazi kabisa kuwa wanunuzi hawatoki hewani, Zaidi ya 80% ya wanunuzi au watumiaji wa Huduma unayotaka kuianzisha ni watu wanaokuzunguka na wale mnaofahamiana vizuri.
 Marafiki zako, walimu wako, wanafunzi wenzako ndio ambao watanunua bidhaa yako au kutumia Huduma zako na kukuletea na Wateja wengine pia. Hawa hawa ndio watakusaidia kuvuka changamoto mbalimbali utakazokumbana nazo. Na hii ndio hali ya dunia ilivyo kwa sasa. Mtu ukiwa na fursa mara nyingi utampa fursa hiyo mtu mwingine katika mtandao wake. Tengeneza mtandao wako kwanza kabla ya kujiingiza katika ujasiriamali. Kazi kubwa uliyo nayo ni kutafuta namna ya kuwa sehemu ya mtandao wa watu wanaoweza kukusaidia kufika mbali zaidi katika biashara yako.

5. JIZOEZE KUFANYA KAZI MUDA MREFU. (Masaa 80 hadi 100 kwa wiki)
Kama umeajiriwa ni rahisi sana kujisahau na kudhani hali itaendelea kuwa hivyo pale utapojikita katika ujasiriamali moja kwa moja. Ujasiriamali hauna masaa maalumu ya kazi. Unaweza ukapiga kazi siku saba za wiki. Hususani katika kipindi cha mwanzo, ni muhimu sana kutumia muda mwingi uwezavyo katika biashara yako ili kuhakikisha inakua vizuri. Kujiandaa na hili ni vema ukaanza kujizoesha kufanya kazi kwa masaa marefu. Kama umeajiriwa basi fanya kazi overtime. Kama ni mwanafunzi basi tafuta kaajira cha ziada kama hali inaruhusu au ongeza muda zaidi katika masomo yako. Hii ni ili kujenga zaidi uwezo wa kufanya kazi kwa bidii ili utakapojikita katika ujasiriamali usikate tamaa kirahisi baada ya kuona masaa ya kazi ni mengi.

6. FANYA UTAFITI.
Mojawapo ya vitu ambavyo vimefanya wengi washindwe kujiingiza katika ujasiriamali au kuingia katika ujasiriamali na kuambulia patupu ni ukosefu wa taarifa sahihi. Na taarifa sahihi hazipatikani sehemu yoyote tofauti na kufanya utafiti wewe mwenyewe kwa kupitia njia mbalimbali.
Kuna kipindi fulani niliwahi kutumia wa kiingereza unaosema “Information is Power” yani “Kujua jambo ni Nguvu”. Kila kitu unachokiona hapa duniani kilianza na taarifa kwanza, kiti hicho ulichokalia kilianza na taarifa au ufahamu wa namna ya kutengeneza kiti hicho kwanza n.k. Kila siku utasikia watu waliofanikiwa wakiongelea jinsi walivyoona fursa ya kuanzisha biashara flani. Unadhani walionaje hiyo fursa? Utafiti. Utasikia wengine wakisema baada ya muda flani wakaongeza bidhaa kutokana na uhitaji wa bidhaa hiyo. Unadhani walionaje uhitaji huo? Utafiti. Utasikia wakisema wamefanikiwa kuongeza mauzo baada ya kutumia mbinu flani ya kujitangaza. Wamejuaje kujitangaza kwa mbinu husika kunaweza kuwasaidia? Utafiti. Kuwa mtafiti ujue mambo ya muhimu yanayoendelea katika eneo la ujasiriamali na hutakosa fursa za kuingiza kipato milele.

7. TAMBUA UBUNIFU NA UWEZO WAKO BINAFSI.
NI dhahiri kuwa vipo vitu ambavyo wewe binafsi peke yako ndio unaweza kuvifanya vizuri zaidi. Hebu vitu hivyo vione kama Fursa na uvifanye kuwa biashara.
Tambua uwezo wako ni nini na ukishafanya hivyo unaweza kujenga biashara yako kwa kuzingatia hili ili uwe na uwezekano mkubwa zaidi wa kufanikiwa. Lakini pia chunguza aina mbalimbali za biashara uone wapi patakufaa. Usiseme unataka kuwa mkulima kama hauko tayari kujifunza kuanzia bei za pembejeo hadi jinsi ya kupanda. Chagua biashara ya kufanya kutokana na utayari wako wa kuifanya biashara hiyo kwa bidii ili ufikie mafanikio. Ukienda kichwakichwa utaishia kuambulia hasara tu. Jitambue kwanza!

8. TAFUTA NGUVU NA UJIANDAE.
Ki ukweli ni kwamba kabla hujaanza kufanya jambo lolote ni lazima ujipange, jenga msuli, Ongeza pumzi kwanza. Ninachotaka kusema ni hivi, jitahidi kujiweka katika kazi au majukumu ambayo yanahitaji kukamilika ndani ya muda maalumu ili kila kitu kiende sawa. Ukifanya hili utakuwa unajijengea uwezo wa kuhimili mikikimikiki katika biashara. Hii ni kwa sababu mara nyingi katika ujasiriamali unahitaji kupangilia vizuri vitu vyako ili ufanikiwe lakini pia uwe na uwezo wa kufanya kazi kubwa ndani ya muda mdogo. Jipangie majukumu wewe mwenyewe na ujipe muda wa kuyakamilisha kwa wakati. Kwa kuwa tayari ulishakuwa na majukumu kama haya ukiwa kazini au kwingineko (mfano shuleni) basi kuna uwezekano mkubwa utafikia mafanikio haraka zaidi.

>Ikiwa kweli kwa moyo wako wa dhati unahitaji kuwa mjasiriamali zingatia sana mambo niliyoyataja hapo juu na bila shaka ujasiriamali wako utakuwa na mafanikio makubwa ..,

Ndugu msomaji huu ni UTANGULIZI TU! Katika kiunga chetu kinachoenda kwa Jina la TAA 7 ZA MJASIRIAMALI. Kati ya vitu nilivyovitaja hapo juu zaidi ya 75% vinadai utayari wako wa KUJIFUNZA! Nami ni mwenzako katika kujifunza nitahakikisha kila nilichijifunza nakushirikisha, si kwingine ni hapa hapa NGWAKWA UFANISI.
KARIBU SANA.

LUCAS ROBERT
+255764075392
+255713056903
lucastrngwakwa@gmail.com

"Live an inspired Life".