HITAJI LA TATU: ARDHI
Mjasiriamali hutumia rasrimali asilia ili kuweza kufanya uzalishaji na kujiingizia kipato. ARDHI Ni mojawapo ya rasrimali asilia ambazo mjasiriamali huzitumia ili kujiingizia kipato. Kwa ufupi hakuna shughuli ya kijasiriamali ambayo inaweza kufanyika pasipokuwa na mchango wa Ardhi.
Ardhi hujumlisha udongo, mito, maziwa, miti, milima,misitu, mvua na madini yaliyo ndani na juu ya uso wa nchi.
Ardhi ni zawadi ya asili ambayo Mungu ametupatia ili tuweze kuitumia kwa ajili ya uzalishaji.
Hivyo basi mjasiriamali ni lazima atambue na kukiri umuhimu wa ardhi katika shughuli zake za ujasiriamali, Na kwa kulitambua hilo ni muhimu sana kwa mjasiriamali kumiliki hata kipande kidogo cha ardhi ili aweze kuwa na uhuru wa kuamua namna ya kuitumia kwa ajili ya uzalishaji.
KWA NINI MJASIRIAMALI AMILIKI ARDHI?
1.Ardhi ni chanzo cha mtaji.
Ardhi ni raslimali isiyohamishika, Na kwa sababu hiyo ikiwa unamiliki ardhi utakuwa na uwezo wa kupata mkopo kwa urahisi ili uweze kuendeleza wazo lako la ujasiriamali. Ardhi inaweza kutumika kama dhamana kwa mkopaji na baadaye atakapokwisha lipa ule mkopo wake Ardhi yake itabaki kuwa yake bila kushuka thamani kwa sababu ni mali isiyohamishika.
2. Ardhi ni chanzo cha fursa kwa mjasiriamali.
Ardhi inaweza kutumiwa na mjasiriamali kutengeneza fursa mbali mbali ambazo atazitumia kwa ajili ya ujasiriamili- kuanzia fursa ndogo mpaka fursa kubwa.
Zifuatazo ni baadhi ya fursa zinazoweza kupatikana kwenye Ardhi.
(a) Ufugaji.
Ardhi unayomiliki unaweza kuitumia kwa ajili ya ufugaji. Ufugaji wa wanyama kama vile Ng'ombe, mbuzi na kondoo. Pia unaweza kutumia Ardhi kwa ajili ya ufugaji wa ndege kama vile kuku, Njiwa, kware, na kanga. Kadhalika pia ufugaji wa wadudu kama nyuki na vipapeo vyote hivyo huhitaji Ardhi. Swala moja tu la ufugaji linaweza kutumia ardhi kwa namna mbalimbali kutegemea na ukubwa wa Eneo na matamanio ya mmiliki.
(b) Utalii na burudani.
Mjasiriamali anaweza kutumia ardhi yake kama sehemu ya utalii burudani na mapumziko.
Katika hili mjasiriamali anaweza kuweka vivutio mbalimbali kama maua mazuri, miti mizuri, mandhari za kupendeza na ikiwa anauwezo mzuri hata wanyama na ndege ambapo watu wataweza kulipa kiasi fulani cha fedha ili waweze kujipumzisha na kuburudisha akili kwa vitu vya asili vinavyopatikana katika eneo husika. Siyo lazima pawepo na vitu vya gharama kubwa sana, panaweza kuwepo na viti vya miti, mawe na kadhalika, njia zilizochongwa vizuri, picha zilizochorwa kwenye mawe au miti na vitu vingine vinavyofanana na hivyo vikiwa na uasili wake.
(b) Uvuvi
Katika ardhi mjasiriamali anaweza kuendesha shughuli za uvuvi kwa kutengeneza mabwawa ya samaki na kuanza kufuga samaki. Ufugaji wa samaki hauhitaji gharama kubwa sana kama zilivyo aina zingine za ufugaji. Katika nyakati hizi soko la samaki linazidi kupanda na muda si mrefu shughuri hii itajipatia umaarufu mkubwa na faida kubwa kutokana kuongezeka kwa mahitaji ya samaki kila uchwao .
(d) Biashara na viwanda vidogo kwa vikubwa.
Ardhi pia inaweza kutumika kea shughuli za biashara pamoja na viwanda vidogo vidogo.
Ardhi ambayo inafaa kwa ajili ya shughuli za biashara ni lazima iwe inafikika kirahisi na watu wa aina zote, mtembea kwa mkuu, mwendesha baisikele na mwenye gari. Pia Ardhi kwa ajili ya biashara haina budi kuwa maeneo safi, yanayoonekana na watu na rafiki kwa watumiaji wa bidhaa yako. Ardhi kwa ajili ya viwanda ni lazima iruhusu upatikanaji wa malighafi pamoja utokaji wa bidhaa kuwafikia watumiaji bila kupuuza maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika kuhusu kusudi la eneo husika.
(e)Makazi- Nyumba za kuishi
Mjasiriamali pia ni lazima atambue umuhimu wa kumiliki ardhi yake binafsi kwa ajili ya makazi yake. Hii itampunguzia kero na upotevu na matumizi mabaya ya fedha kwa kupanga. Kumiliki ardhi kwa ajili ya makazi pia kutaruhusu utulivu wa akili na moyo na kuruhusu kutulia katika shughuli anayoifanya bila usumbufu wa kuhamahama.
(f) Huduma za kijamii - Shule, Hospitali.
Ardhi pia inatoa fursa kwa mjasiriamali kuanzisha huduma za kijamii kama vile shule na hospitali. Huu pia ni uwekezaji ambao mjasiramali anaweza kuufanya ili kujiingizia kipato. Unapoanzisha huduma hizi za kijamii siyo lazima uwe na majengo mengi, unaweza kuanza na jengo moja au mawili na ukafuatilia tu taratibu za mamlaka husika ukaanza na kupanuka kwa kadri unavyoenda.
(g) Kutunza na kuhifadhi mali.
Ardhi inaweza kutumika kutunza au kuhifadhi mali za watu wengine. Kama mjasiriamali unamiliki ardhi ambayo huna uwezo wa kuiendeleza hivi karibuni na ipo eneo linalofikiwa na watu wengi hasa walio na usafiri au magari unaweza pia kuitumia kama sehemu ya kuegesha magari, biashara hii haihitaji mtaji mkubwa sana, Inahitaji uadilifu na Uhakika wa usalama. Katika hili pia unaweza kujenga ghala na kulikatia bima kisha ukaanza kuhifadhi mazao na kila utakayemuhifadhia mnaweka makubaliano ya kumkata asilimia fulani ya mazao hayo baada ya muda fulani, hii pia itakuwezesha kutumia Ardhi yako kuingiza kipato.
>>> Hizo ni fursa chache sana ambazo zinapatikana katika Ardhi, Lakini zipo nyingi zaidi ya hizo nilizotaja. Katika nchi zilizoendelea mtu ambaye anamiliki ardhi ndiye ambaye ana uwezekano wa kufanikiwa kuliko mtu yoyote.
Uwekezaji katika Ardhi ndiyo uwekezaji wenye faida kubwa kulika zote kwa sababu Ardhi huwa inapanda bei kila kunapokucha haijalishi ni muda gani umeitumia.
*** Hivyo basi mpendwa msomaji napenda kutumia nafasi hii kukuomba uone umuhimu wa kumiliki Ardhi kabla hujaingia katika ujasiriamali.
**Ardhi ni hitaji muhimu sana kwa mjasiriamali, ipe uzito**
Lucas Robert.
+255764075392
lucastrngwakwa@gmail.com.
"LIVE AN INSPIRED LIFE"


